Thursday, October 17, 2013

Zaidi ya wanariadha 2000 kushiriki Rock City Marathon 2013

ZAIDI ya wanariadha 2000 wanatarajia kushiriki mbio za mwaka huu, za awamu ya tano za Rock City, zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza mwezi Oktoba tarehe 27, kamati ya maandilizi imesema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa kamati ya maandilizi ya mbio za Rock City mwaka huu, Bw. Mathew Kasonta alisema mwenendo wa usajili unaonyesha matumaini makubwa na kuongeza kuwa inatarajiwa kushika kasi zaidi katika wiki hii ya mwisho ambapo washiriki wanategemewa kuongezeka kufikia 2000 kwa mwaka huu.  

“Tunayo faraja kubwa kuona usajili unaendelea vizuri. Watu wengi wameshajitokeza kujisajili na kuchukua fomu wenyewe, na wengine wameshalipia fomu zao kupitia Airtel Money. Japokuwa usajili unaendelea, kwa mpaka jana, takwimu niliyo nayo inaonyesha kuwa wale waliochukua fomu zao wamefikia washiriki 531, wakati wengi waliotumia Airtel Money kulipia watachukua fomu zao wakati wowote kupitia vituo vifuatavyo; 

Makao Makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam, Maduka ya Airtel Dodoma, Arusha, Mwanza, Zanzibar na Mbeya,” alisema. Mratibu wa mbio hizo alisema usajili bado unaendelea na fomu zinapatikana katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International jijini Dar es Salaam, viwanja vya Nyamagana mkoani Mwanza na ofisi zote za michezo za wilaya mkoani Mwanza.

Kasonta alibainisha kuwa wanariadha kutoka nje wameonyesha nia yao ya kushiriki kwa kutuma maombi yao kupitia Chama cha Riadha Tanzania (RT) – ambacho kitahakikisha washiriki wote wa kutoka nje wanafuata taratibu zote za kisheria kabla ya kushiriki.

“Tumeshapata simu kutoka kwa washiriki kutoka nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), pamoja na washiriki ambao ni raia wa Australia, India, Canada na Amerika, wanaotaka kushiriki mbio hizi. Sababu tunafanyakazi kwa ukaribu na RT, tumeamua kuwa RT watahakikisha washiriki kutoka nje wanafuata taratibu zote kabla ya kushiriki ili kuifanya Rock City Marathon ifikie viwango vilivyowekwa kimataifa,” alisema Kasonta. Mbali na washiriki ambao tayari wamechukua fomu zao, Kasonta alisema makampuni mbali mbali, wafanyabiara, taasisi na watu maarufu wamethibitisha kuleta timu zao ili kushiriki mbio za kilometa 5 ambazo ni maalum kwa wafanyakazi.

Mratibu alisema kupitia udhamini wa NSSF, Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Airtel kupitia Airtel Money, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications, Continental Decoders na Umoja Switch, kamati imeboresha zawadi zitakazoshindaniwa na kualika kikundi cha Sanaa cha Bujora kitakachokuwepo kunogesha tukio hilo.

“Rock City Marathon ambayo kwa miaka mitano sasa imekuwa ikiandaliwa na kampuni ya Capital Plus International Ltd, kwa miaka mingi imekuwa ikibeba kauli mbiu ya “Tukuze utalii wa ndani kupitia michezo.” Kwa kutambua hilo, katika mbio za mwaka huu, tutaburudishwa na kikundi cha Sanaa cha Bujora ambacho kimeonyesha kuwa kikundi bora zaidi kwa kuonyesha utamaduni wa kitanzania kupitia dansi,” alisema.

Mbio za mwaka huu zinavipengele vitano ambavyo ni kilometa 21 kwa wanaume na wanawake, kilometa 5 kwa wafanyakazi kutoka katika makampuni, kilometa 3 kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, kilometa 3 kwa wazee kuanzia miaka 55 na zaidi na kilometa 2 kwa watoto kuanzia umri wa 7 mpaka 10.

PICHA 7 ZA MAZISHI YA MAMA UFOO SARO ALIYEUAWA KWA RISASI NA MKWEWE

Mtoto wa mwandishi na mtangazaji wa kituo cha ITV,Ufoo Saro,Alvis Anthery akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza la marehemu Bibi yake Anastazia Saro aliyezuikwa jana katika makaburi ya kanisa la Urara wilayani Hai.
Umati wa waombolezaji waliojitikeza katika kuaga mwili wa marehemu Anastazia Saro aliyezikwa katika makaburi ya kanisa la Urara wilayani Hai.
Msemaji wa familia ya Saro,Allelio Swai akitoa maelezo ya familia wakati wa ibada ya kumuombea marehemu Anastazia Saro.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Anastazia Saro likiwekwa kaburini.
Mkuu wa jimbo la Hai,Aminirabi Swai akiongoza ibada ya maziko katika makaburi ya kanisa hilo na kisha kuweka shada la maua katika kaburi la marehemu Anastazia Saro.
mwakilishi wa serikali katika maziko ya marehemu Anastazia Saro ,mkuu wa wilaya ya Hai Novatus Makunga akiweka shada la Maua katika kaburi.
Mtoto Alvis Anthery akiweka shada la maua katika kaburi la Bibi yake marehemu Anastazia Saro.(picha na Dixon Busagaga)

Na Dixon Busagaga waglobu ya jamii Moshi

VILIO,simanzi na hali ya huzuni jana vimetawala kwa mamia ya wakazi wa kijiji cha Shari, Machame wilayani Hai waliojitokeza kuuaga mwili wa marehemu ,Anastazia Saro (56),mama mzazi wa Mwanadishi na Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV,Ufoo Saro.

Wakazi hao wakiwemo wale waliotoka maeneo mbalimbali ya miji ya Moshi,Arusha na Dar es Salaam baadhi yao walionekana wakiangua vilio huku wengine wakipoteza fahamu muda mfupi baada ya jeneza lililobeba mwili wa marehemu kuingizwa kanisani.

Hali ilikuwa ya Simanzi zaidi wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa waombolezaji wakipita mbele ya jeneza ambapo ililazimika kuwepo na watu maalumu ambao walikuwa na jukumu la kutoa huduma ya kwanza kwa baadhi ya ndugu walioshindwa kujuzuia.

Hali kama hiyo ili rejea kwa mara nyingine tena pale msemaji wa familia Allelio Swai akitoa maelezo ya namna marehemu alivyo uawa na hali aliyokutwa nayo mara baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari.

Akitoa maelezo ya wasifu wa marehemu aliyefanyiwa ibada ya mazishi katika Kanisa la Urara lililopo chini ya Jimbo la Hai la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Swai alisema marehemu Anastazia Saro alifikwa na mauti hayo baada ya kupigwa risasi na mkwewe Anthery Mushi ambaye alikwenda nyumbani kwa mama huyo eneo la Kibamba CCM,nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema taarifa ya madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inaonyesha,Anastazia Saro alifariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi tano katika mwili wake.

Swai aliomba kufanyika maombi kwa ajili ya Ufoo aliyelazwa katika hosptali ya Muhimbili ambako anapatiwa matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa hali iliyolazimu madaktari kumpa muda mrefu wa mapumziko.

“ Ufoo taarifa ya madaktari inaonesha alichanika utumbo mkubwa na kiasi utumbo mdogo,lakini tunashukuru hali ya Ufoo inaendelea kuimarika ,lakini maombi yenu yanahitajika ili aweze kurejea katika hali yake ya zamani ,na aweze kulitumikia taifa kwa kuhabarisha “alisema Swai.

Kwa upande wake,baba mdogo wa Ufoo Saro, mzee Eshikaeli Saro, akizungumza katika ibada ya mazishi kanisani hapo,alisema familia na kanisa imepoteza mtu aliyekuwa kiungo muhimu kati ya jamii na kanisa.

“Mama alikuwa ndiye mpambaji wa madhabahu ya kanisa ,na alihakikisha kanisa linakuwa katika hali ya usafi kabla ya ibada na hata pale wanakwaya walipokuwa na mazoezi ya kutwa hapa kanisani alihakikisha wanapata chakula”alisema Saro.

Alitoa shukrani kwa Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Dk.Regnald Mengi,mkurugenzi mtendaji wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile pamoja na wafanyakazi wote wa makampuni hayo kwa kuifanya familia hiyo iweze kumfikisha marehemu Machame na kuzikwa.

Marehemu Anastazia Saro, aliuawa baada ya mkwewe kufika nyumbani kwake Kibamba CCM akiwa na mzazi mwenzie Ufoo kwa lengo la kusuluhishwa kile kinachodaiwa ni ugomvi uliokuwa ukifukuta kati ya wawili hao.

Tukio hilo lilitokea alfajiri ya Jumapili ya Oktoba 13 mwaka huu, huku mwanae Ufoo Saro ambaye ni Mwandishi na Mtangazaji wa ITV, akijeruhiwa vibaya kwa risasi mbili baada ya kutokea ugomvi kati yakena mzazi mwenzie Anthery Mushi ambaye hata hivyo na yeye alijiua kwa kujipiga risasi baada ya tukio hilo.

MWINYI ATAKA WAGANGA WA TIBA ASILI KUSHIRIKIANA NA WATAFITI

NA MAGRETH   KINABO – MAELEZO
 
WAZIRI wa Afya na  Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi amewataka  waganga  wa tiba asili washirikiane na wataalamu wa utafiti ili kuwezesha upatikanaji wa dawa bora na salama.

 Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri huyo wakati akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya siku ya tiba ya asili ya mwafrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Agosti 31, lakini mwaka huu hayakufanyika kutokana na uhaba wa fedha. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika mwakani kipindi  katika hicho.

“ Tanzania tunayo mitidawa mingi na mingi haijafanyiwa kazi katika utafit na kuweza kubaini uwezo wa kutibu magonjwa mbailmbali tatizo lililopo ni jinsi gani mitidawa hiyo inweza kufanyiwa utafiti na kuwa dawa bora na salama kwa watumiaji kwa kuziwekea mifumo ya huduma za afya ili kila mwenye kuhitaji aweze kuzipata,” alisema Dk. Mwinyi .

 Dk. Mwinyi aliwataka waganga hao kushirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)  na  Taasisi  ya  Utafiti wa Dawa za Asili iliyokpo katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi  Shiriki- (MUHAS).

 Aliongeza kuwa waganga wote wa tiba asili na tiba ya kisasa wanatakiwa kufanya kazi kwa kuelewana ili kuwezesha kupata taarifa za awali kabla ya utafiti kamili kufanyika.

 Aliitaja kauli mbiu ya maadhimisho hayo kuwa ni ‘ Tiba Asili : Utafiti na Maendeleo’ kuwa inalenga kutoa majukumu  kwa waganaga wa tiba asili na tiba mbadala katika sula zima la utafiti. Pili inatoa changamoto juu ya uendelezaji wa taarifa za utafiti wa mitidawa katika kutafuta dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali.

 Aidha aliwahimiza waganga wa tiba asili kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na huduma za afya.

Swahili Fashion Week ya Sita yazinduliwa rasmi jijini Dar

Meneja wa Swahili Fashion Week Washington Benbella (Katikati)akizungumzia tarehe za Swahili Fashion Week 2013.
IMG_0550
Meneja Maboresho Swahili Fashion Week, Hamis K Omary akizungumzia uboreshwaji wa Swahili Fashion Week 2013.
IMG_0567
Meneja Masoko wa EATV na Ea RadioHappy Shame(kulia)  akizungumzia mipango ya EATV na Radio juu ya Swahili Fashion Week mwaka huu.
IMG_0579
Mratibu wa Masoko na Mauzo kutoka Hoteli ya Golden Tulip Bi. Catherine Lumbanga akizungumzia jinsi hoteli yao inafurahi kushirikiana Swahili Fashion Week kwa mwaka wa pili mfululizo.
IMG_0599
Bw. Honest Arroyal,Mratibu wa Mitindo Swahili Fashion Week (wa pili Kushoto) akizungumzia ujio mpya wa Swahili Fashion Week 2013.
IMG_0602
Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka sehemu mbalimbali wakifuatilia uzinduzi huo. 

Maonesho ya sita ya Swahili Fashion Week yatafanyika Golden Tulip Hotel kuanzia tarehe 5 mpaka 8 Desemba 2013, Dar Es Salaam, Tanzania.
Swahili Fashion week 2013 itakusanya wabunifu 40 kutoka ndani na nje ya Tanzania ili kuonesha mitindo yao, yenye kwenda na wakati na kutegemewa kushika soko la Afrika Mashariki mwaka 2014.
“Swahili Fashion Week mwaka huu ina lengo la kuifikia jamii zaidi, na kukuza vipaji katika tasnia ya mitindo. Ni zaidi kuhusu kuthamini wabunifu wa kwetu na kuwatengezea jina,huku tukiwapeleka ngazi za juu zaidi kila mwaka” Akizungumza Bw. Washington Benbella, Meneja wa Swahili Fashion Week
Ukiwa ni mwaka wa 6 wa Swahili Fashion Week, Katika mashindano ya wabunifu wanaochipukia, Waandaaji wamependekeza dhima ya mwaka huu (theme) “Evolution” ambayo inawataka wabunifu chipukizi hao kubuni mavazi yanayoashiria mabadiliko, si lazima upya, ila yenye muonekano wa kitofauti na mzuri.
“Tunasisitiza jamii iunge mkono tasnia ya mitindo na kuvaa mavazi ya kikwetu, hasa kwa Tanzania. Vipaji vya nyumbani vinahitaji kukuzwa ili kufikia majina yanayotambulika duniani katika tasnia hii. Hisani huanza nyumbani, na ndio maana tunategemea kampuni pamoja na mashirika mbali mbali kusaidia tasnia ya mitindo” Hamis K Omary, Meneja Masoko Swahili Fashion Week.
Swahili Fashion week imedhaminiwa na EATV, East Africa Radio, Golden Tulip Hotel, Eventlites, Push Mobile, BASATA (Baraza la Sanaa la Taifa), Ultimate Security, Global Outdoor Ltd na 361 Degrees.

Rwanda, Tanzania zinautawala bora zaidi EAC

Perezida-Paul-Kagame-na-Jakaya-Kikwete-muri-Nyakanga-2012-i-Kigali
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Rwanda Paul Kagame.(Picha na Maktaba).

Tasisi ya Mo Ibrahim juu ya Utawala Bora Afrika, imebaini nchi za Rwanda na Tanzania kuwa nchi zenye utawala bora zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kati ya nchi 52 za kiafrika.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatatu, Rwanda imepata wastani wa asilimia 57.8 ikiwa ni zaidi ya wastani wa kiafrika wa asilimia 51.6.
Hii inamaanisha kwamba nchi hiyo imeboresha utawala bora kwa zaidi ya asilimia 10.9 tangu mwaka 2000, ikiwa nafasi ya kwanza kwa nchi za Afrika mashariki ikifuatiwa na Tanzania iliyoshika nafasi ya 17 barani Afrika kwa kupata asilimia 56.9 huku Uganda ikiwa ya tatu ECA kwa kuwa ya 18 kwa kupata asilimia 56. Kenya imekuwa ya 21 na kushika nafasi ya nne kwa kupata asilimia 53.6 huku Burundi iliyopata asilimia 43.8 ikishika nafasi tano kwa EAC.
”Rwanda imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka tangu mwaka 2000, ikiwa ni maboresho makubwa zaidi katika nyanja ya Maendeleo ya Binadamu hususa ni katika sekta ya elimu na afya,” ripote ilisema.
Mauritania imeshika nafasi ya kwanza katika Afrika kwa kupata asilimia 82.9 ikifuatiwa na Botswana aliyopata asilimia 77.6 ambapo Cape Verde imeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 76.7. barani.
Ripoti hiyo imebaini kwamba asilimia 94 ya nchi za Afrika ikiwemo Rwanda watu wake wanaishi katika nchi ambazo zimeboresha kwa ujumla masuala ya utawala bora tangu mwaka 2000.
Asilimia sita ya watu wanaoishi kwenye nchi ambazo kiwango cha utawala bora kimeshuka tangu mwaka 2000 ni pamoja na nchi za Guinea-Bissau, Madagascar, Somalia, Libya na Mali.
Taasisi hiyo ya Mo Ibrahim pia hutoa tuzo kwa viongozi bora barani Afrika.Hata hivyo tuzo hiyo haijatolewa kwa mara ya nne sasa.
Tuzo hiyo hutolewa kwa kiongozi wa Afrika aliyechaguliwa kidemokrasia aliyeonesha kwa vitendo uongozi bora,kutumikia muhula wake wa uongozi na kuachia ngazi miaka mitatu iliyopita.

Tuesday, February 12, 2013

OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI YAUNGANISHWA KWENYE MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kukamilika kwa mradi wa kuiunganisha ofisi hiyo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, mradi uliofanywa kwa ufanisi na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa gharama ya shilingi milioni 477.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akipokea cheti cha kukamilika kwa mradi wa kuiunganisha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kwa Bw. Kisamba Tambwe (kulia) Meneja wa njia za Mawasiliano za nje kutoka Kampuni ya simu Tanzania.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh (katikati mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo na viongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL leo jijini Dar Es salaam.

Na. Aron Msigwa -MAELEZO. Dar es salaam.
Ofisi yaTaifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano wa matumizi ya barua pepe na intraneti utakaoiwezesha ofisi hiyo kutuma na kupokea taarifa za utendaji kwa haraka kufuatia kukamilika kwa mradi wa kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati wa makabidhiano ya mradi huo uliofanywa na kampuni ya Simu Tanzania, Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh amesema kuwa mradi huo utaiwezesha ofisi yake kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya ofisi kupitia mfumo wa intaneti.

Amesema mradi huo ambao kwa sasa umeanza kwa kuziunganisha ofisi 12 za mikoa mbalimbali utaleta mabadiliko makubwa katika nyanja nzima ya upashanaji habari na utawawezesha watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za serikali kupata mawasiliano kwa kwa haraka na usalama zaidi kupitia makao makuu ya ofisi hiyo.

Amesema mkongo wa taifa utaiwezesha ofisi hiyo kumiliki na kudhibiti taarifa mbalimbali zinazotumwa kwa kuwatumia wataalam wa Tehama wa ndani huku akibainisha kuwa mfumo huo mpya utawazuia watumishi wa ofisi hiyo kutumia mifumo ya kawaida ya barua pepe na mitandao hatarishi inayoweza kuleta madhara kwenye taarifa muhimu za serkali.

" Mradi huu umekamilika wakati muafaka kwa sababu utatuwezesha kupunguza gharama, kumiliki na kudhibiti sisi wenyewe taarifa zetu za kiutendaji za kila siku kupitia wataalam wa Tehama tulionao katika ofisi zetu na kuondoa kabisa mfumo uliokuwepo wa kubeba taarifa mikononi kutoka eneo moja hadi jingine" amesema Utouh.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali nchini kujenga uwezo wa uimarishaji wa miundombinu za shughuli za Ukaguzi na utendaji na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia mfumo wa kompyuta huku akifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Tanzania kwa kipindi cha miaka 6 ni wakaguzi wa Umoja wa mataifa ukaguzi unaofanywa katika miji mbalimbali duniani.

Utouh amebainisha kuwa ofisi yake sasa itaweza kufanya mikutano ya kiutawala moja kwa moja na ofisi za mikoani kupitia mfumo mpya wa mawasiliano wa mtandao (video conference) na kuwataka watumishi wa ofisi hiyo kuutumia ipasavyo mfumo huo kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake Meneja wa njia za mawasiliano ya nje wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Bw. Kisamba Tambwe akikabidhi mradi huo amesema kuwa kampuni hiyo imetekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa ili uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.

Amesema TTCL itaendelea kuhakikisha kuwa ofisi 12 za mikoa iliyouganishwa kwenye Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa zinakuwa na usambazaji salama wa taarifa kutoka eneo moja hadi jingine.